KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Tuesday, April 19, 2016

AMIN SALMIN WA T-MOTO AKANA KUWA NA BIFU NA MZEE YUSSUF


MKURUGENZI wa kikundi cha taarab cha Tanzania Moto, Amin Salmini, amesema hana ugomvi wala bifu na Mkurugenzi wa kikundi cha Jahazi, Mzee Yussuf.

Hata hivyo, Amin amekiri kuwepo kwa upinzani wa kibiashara kati yao, lakini umelenga zaidi katika kazi na kuinua biashara ya muziki huo.

Amin alisema ni kweli nyimbo nyingi zinazoimbwa na mkewe, Jokha Kassim, zimelenga kumpiga vijembe mke wa Mzee Yussuf, Leila Rashid, lakini ni katika ushindani wa kibiashara.

"Ni kweli kuna upinzani wa kibiashara kati yangu na Mzee Yussuf, lakini ni upinzani wa kibiashara uliopo kati yetu, ni upinzani wa kikazi zaidi.

"Halafu mimi huwa simjibu Mzee Yussuf, huwa najibu shairi. Ninavyofanya vile, nalenga kuonyesha ubora wangu katika kutunga nyimbo, si vinginevyo,"alisema Amin.

Mtoto huyo wa Rais wa zamani wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, alisema ukimya wa kundi la Tanzania Moto, umetokana na hali yake kiafya kutokuwa nzuri.

"Watu wengi wanadhani kuwa siasa ndio imenifanya niwe kimya, lakini ukweli ni kwamba siasa haiwezi kunipoteza katika muziki wa taarab.

"Hii ilikuwa ni kazi maalumu katika uchaguzi tu na sasa umekwisha, hivyo najipanga kurudi Dar es Salaam, kuendelea na mapambano ya kuinyanyua T Moto,"alisisitiza Amin.

Mkurugenzi huyo amekiri kuwa bado kundi lake halijapata mafanikio makubwa kutokana na muziki huo kwa vile bado halijasimama vizuri.

Alisema hadi sasa, kundi hilo limefanikiwa kurekodi albamu mbili, ikiwemo Domo la Udaku, ambayo ilishika chati katika vituo vya redio na televisheni nchini.

Amin alisema pia kuwa, si kweli kwamba majibizano ya nyimbo katika muziki wa taarab yanaweza kujenga chuki na uhasama kati yao. Alisema muziki wa taarab umelenga zaidi katika kujibizana.

"Kwa mfano, Khadija Kopa na marehemu Nasma Kidogo walikuwa wakiimba nyimbo za kujibizana, lakini hawakuwa na uhasama zaidi ya kujiongezea mashabiki.

"Vivyo hivyo hata mimi sioni kama kwa kufanya hivyo ninapoteza mashabiki, isipokuwa nimekuwa nikijiongezea mashabiki kutokana na tungo zangu,"alisisitiza.

Amin alikiri kuwa ni kweli kuwa kwa sasa wanajiandaa kurekodi wimbo mpya, ambao umelenga kuujibu wimbo mwingine wa Jahazi. Aliutaja wimbo huo kuwa ni 'Hakuna kuomba poo'.

Alisema wamefanya hivyo kutokana na ukweli kwamba Jahazi ndilo kundi lililopo juu kimuziki hivi sasa, hivyo si rahisi kufanya ushindani na kundi lingine zaidi ya Jahazi.

"Ukitaka ushindani katika muziki wa taarab, ni lazima ushindane na kundi lililo juu yako,"alisema.

Amin alisema katika albamu yao mpya wanayotarajia kuitoa hivi karibuni, itakuwa na nyimbo tano na wanatarajia kuwa na msanii mmoja mpya, ambaye hakutaka kumtaja jina lake.

Alisema kundi hilo litaendelea kuwa chini ya Jokha Kassim na kwa wapiga ala, watakuwa chini ya Omary Kisila.

No comments:

Post a Comment