KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Saturday, February 14, 2015

ISHA MASHAUZI AIBUKA NA KITU KINGINE KIPYA


Wala hakosei kusema ‘kujua kazi ni raha’.

Isha Mashauzi anakushukIa tena kivingine na wimbo mpya kabisa “Nimpe Nani” unaodhihirisha kuwa anaijua vema kazi yake.

Hii ni ‘single’ yake ya pili nje ya taarab ukiacha ule wa kwanza “Nimlaumu Nani” uliopigwa katika miondoko ya rhumba.

“Nimpe Nani” ni wimbo unaoelea kwenye miondoko ya zouk rhumba lakini ukikolezwa kwa mbali na vionjo vya mduara.

Wimbo huo wa dakika tatu na nusu umerekodiwa katika studio za C9 Records chini ya producer C9 Kanjenje.

Kinanda kimepigwa na Kali Kitimoto na C9, magitaa ya bass na solo yamepigwa na Babu Bomba wa Malaika Band.

Sauti zote tamu unazozisikia humo ni za Isha Mashauzi kasoro sehemu ndogo sana isiyozidi sekunde 5 iliyotikiwa na Easy Man.

Tuesday, February 3, 2015

THANIA MSOMALI AJA NA 'HIVI NDIVYO NILIVYO'



MIEZI michache baada ya kujiengua katika kundi la Mashauzi Classic, mwimbaji machachari na mwenye sauti maridhawa ya ndege mnana, Thania Msomali ameibuka na kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Hivi ndivyo nilivyo.

Katika kibao hicho, ambacho kimeshaanza kuteka hisia za mashabiki, Thania anasimulia jinsi alivyo na kwamba yuko tofauti na vile watu wanavyomfikiria.

Thania alianza kung'ara kimuziki alipokuwa katika kundi la Five Stars, baadaye akajiunga na kundi la T-Moto kabla ya kutua Mashauzi Classic, kundi linaloongozwa na Isha Ramadhani 'Mashauzi'.

Binti huyo jamali na mwenye sauti murua na adhimu, anakiri kuwa kipaji chake kiligunduliwa na mpiga kinanda Omary Kisira, ambaye ndiye aliyempika na kumfanya awive kisawasawa.

Thania alijiengua mwenyewe kutoka kundi la Mashauzi Classic baada ya kuona kwa sasa anaweza kusimama peke yake.

Binti huyo amesema kibao hicho ni maandalizi ya ujio wa albamu yake ya kwanza, anayotarajia kuitoa mwaka huu.

Amesema alianza maandalizi ya kutoa albamu mpya muda mrefu uliopita, lengo likiwa ni kutoa kitu kilichokamilika na chenye ladha isiyomithilika kwa utamu.

"Sikukurupuka kurekodi kibao hiki, nilijiandaa vyema ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi ya kutosha,"alisema.

Thania kama msanii mchanga, amekubaliana na changamoto zote atakazokumbana nazo, pia anawasihi wasanii wote kupendana na kusaidiana pale unapoona mwenzako amekwama au anakwenda sivyo, hata mawazo tu.

"Napenda kuwashukuru wale wote waliofanikisha kwa mimi kuwepo hapa nilipo:- Walimu wangu Fikirini Urembo na Kibibi Yahaya, vilevile nitakuwa mwizi wa fadhila kukosa kutoa shukrani zangu kwa walimu wangu waliopita ambao ni Ally Jay, Shaibu wa Mwamvita pamoja na Kali Kiti Moto Mafya.

"Pongezi kubwa ziwaendee Amin Salmin, Mkurugenzi wa T-Moto pamoja na Ismail Suma Ragger, Meneja wa Mashauzi Classic.

Amewaomba wapenzi wote wa taarab kumpokea na wausikilize kwa makini wimbo wake huo ili wajue kaimba nini na zaidi ya yooote, huu ni mwanzo tu, yaani mvua za rasharasha masika inakuja, ni mvua ya mawe kama si elnino.

WAKALI WAO MODERN TARADANSI WAJA NA VIBAO VIWILI VIPYA, MISAMBANO ASHUSHA MOJA KALI



KUNDI jipya la muziki wa taarab la Wakali Wao Modern Taradansi, limeibuka na vibao vingine viwili vipya.

Vibao hivyo, ambavyo tayari vimeshaanza kusikika kwenye vituo mbalimbali vya redio nchini ni Kumbe ndio tabia yake na Jasho la mnyonge hulipwa na Mola.

Kibao cha Kumbe ndio tabia yako kimeimbwa na mwanadada Nasra Shaaban wakati kibao cha Jasho la mnyonge hulipwa na Mola kimeimbwa na kiongozi wa kundi hilo Thabit Abdul.

Akizungumza na mtandao huu wiki hii, Thabit alisema ujio wa vibao hivyo viwili ni maandalizi ya ujio wa albamu yao mpya, inayotarajiwa kutoka hivi karibuni.

Alisema tayari wameshakamilisha vibao viwili na kwamba vingine vitatu bado vipo jikoni na vinatarajiwa kupakuliwa hivi karibuni.

Thabit alisema kama ilivyo kawaida, wamepiga vibao hivyo kwa miondoko ya taarabu ya kisasa kwa lengo la kuwavutia zaidi mashabiki.

Wakati huo huo, mkali wa miondoko ya taarab, Abdul Misambano naye ameibuka na kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Sio mie ni moyo.