KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Friday, December 26, 2014

FIVE STARS YAJA NA TATU MPYA, ISHA MASHAUZI APAKUA SURA SURAMBI




KIKUNDI cha taarab cha Five Stars, ambacho kimezidi kujiimarisha kwa kuwanyakua waimbaji wapya kadhaa, wiki iliyopita kiliingia studio kurekodi vibao vitatu vipya.

Vibao hivyo vipya ni Ubaya hauna soko kilichoimbwa na Mwanaidi Ramadhani, Kishtobe kilichoimbwa na Salha na Sina Gubu kilichoibwa na Mape Kibwana.

Kiongozi wa kundi hilo, Ally J, ametamba kuwa vibao hivyo vitakuwa moto wa kuotea mbali kutokana na kupigwa katika miondoko ya kisasa zaidi.

Wakati huo huo, kiongozi wa kundi la Mashauzi Classic, Isha Ramadhani, ameachia kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Sura Surambi.

Kibao hicho ni utunzi na uimbaji wake Isha Mashauzi na tayari kimesharekodiwa wikiendi iliyopita kwenye studio za Sound Crafters, zilizoko Temeke jijini Dar es Salaam chini ya producer Enrico.

“Sura Surambi” inategemewa kuendelea kumweka juu Isha Mashauzi kwa namna alivyoimba wimbo huo na hapana shaka itatosha kabisa kuthibitisha ni kwanini alistahili tuzo ya mwimbaji bora wa kike wa taarab.

Gita la solo katika wimbo huo limepigwa na Ramadhani Kalenga, besi limepigwa na Rajabu Kondo wakati kinanda kimepapaswa na Kalikiti Moto.

No comments:

Post a Comment