KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Saturday, April 27, 2013

ISHA MASHAUZI 'AUZIWA' KESI YA WIZI


MKURUGENZI wa Mashauzi Classic, Isha Ramadhani ‘Mashauzi’ jana alionja adha ya umaarufu baada ya kusoteshwa kituo cha polisi cha Msimbazi huku kamera za waandishi maarufu zikimsubiri nje ya kituo hicho.
Isha alifikishwa kituoni hapo kwa kuhusishwa na upotevu wa shilingi laki saba uliotokea kwenye duka moja la Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Mmiliki wa duka hilo la nywele, amemfikisha Isha na mwenzake aitwae Halima kituoni hapo akidai alipotelewa na kiasi hicho cha pesa huku msanii huyo akiwa ni wa mwisho kuingia dukani mwake.

Saluti5 ilifika kituoni hapo majira ya 5 za usiku na kukuta waandishi wengi wakimsubiri Isha atoke ili wapate picha, jambo ambalo walifanikiwa licha ya Isha kujitahidi kuwakwepa.
Inaaminika mmiliki wa duka hilo alipiga simu karibu kwa kila chombo cha habari ili waandishi wafike hapo akiamini kuwa jambo hilo litasaidia kumdhalilisha msanii huyo.

Akiongea na Saluti5 muda mfupi baada ya kutoka kituoni hapo, Isha alisema alifika dukani kwa dada huyo Jumamosi iliyopita lakini baada ya kukosa alichokifuata aliingia duka lingine na kuliacha gari lake jirani na duka hilo.
Wakati anarudi kwenye gari lake, wafanyakazi wawili wa duka hilo wakamfuta na kumwambia kuna upotevu wa pesa umetokea.

Isha anasema baada ya mjadala wa muda mrefu  akaawachia namba ya simu na kuwaambia iwapo bado watahitaji ufafanuzi zaidi wawasiliane.
Isha anasema: “Kuanzia Jumatatu alianza kunipigia simu za vitisho na kuniambia atanikomesha na kunidhalilisha.

“Vitisho vilipokithiri, Jumanne jioni nikaenda kituo cha Msimbazi kuripoti juu ya vitisho vyake, lakini kituoni wakaninyima ushirikiano wakaniambia niende Kinondoni ninakoishi.

“Nikawaambia nimekuja Msimbazi kwa vile biashara ya mtu anayenipa vitisho hivyo ipo Kariakoo, lakini bado walikataa kunihudumia.

“Nilirudi nyumbani nikipanga kuwa kesho yake niende kituo cha Oysterbay lakini leo (jana) nikapigiwa simu kutoka Msimbazi kuwa nifike kituoni hapo.

“Nikadhani labda sasa wameamua kunisikiliza, nilipofika kituoni hapo nikawekwa chini ya ulinzi kwa tuhuhuma za wizi wa shilingi laki 7.”

Baada ya kusota kwa masaa kadhaa Isha aliruhusiwa lakini akitakiwa kurudi tena kituoni hapo siku inayofuata (leo).

Watu kadhaa walifika kituoni hapo kumwekea dhamana Isha ambaye aligoma kabisa kuingizwa mahabusu.

Waliofika hapo akiwepo mtangazaji wa Times FM, Dida walifikia hata hatua ya kutaka kulipa pesa hizo lakini Isha alikataa kabisa jambo hilo lisifanyike akidai hii ni aina mpya ya utapeli.

“Haiwezekani duka ambalo lina wafanyakazi wawili na wateja wengi wanaoingia useme mtu fulani kakuibia.

“Kwanza mteja unakuwa nyuma ya kaunta yao na si rahi kujua pesa zilipo, utalivuka vipi hilo kaunta mpaka ufike kwenye pesa bila wahusika kukuona?

“Kwanini wasinikamate muda huo huo na kunipigia kelele za mwizi?” alihoji Isha.
Askari mmoja wa kituo hicho aliiambia Saluti5 kuwa malalamiko ya kesi hiyo yana mushkel na yamekaaa kiujanja ujanja ujanja.

Ameshangaa ni kwanini tukio la Jumamosi liachiwe hadi Jumatano, akashaangaa pia namna waandishi walivyotaarifiwa tukio hilo ndani ya muda mfupi.
IMEHAMISHWA KUTOKA SALUTI 5

Friday, April 19, 2013

SERIKALI ZANZIBAR ILIGHARAMIA MAZISHI YA BI KIDUDE



Na Othman Khamis Ame, OMPR
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kugharamia mazishi ya Gwigi la Sanaa ndani ya ukanda wa Afrika ya Mashariki na mipaka yake Anti Fatma Binti Baraka { Maarufu Bi Kidule } aliyefariki dunia juzi mchana baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Hatua hiyo imekuja kufuatia mchango wake katika kuitangaza sanaa ya Zanzibar nje ya mipaka ya Tanzania hasa kwenye fani ya muziki wa Taarabu asilia na ile ngoma maarufu ya Unyago inayotumika katika sherehe za harusi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akiifariji familia ya Marehemu Bi Kidude wakati wa matayarisho ya mazishi yake hapo Mtaani kwake Rahaleo nyuma ya Kituo cha ZBZ Redio, Rahaleo Mjini Zanzibar.
Balozi Seif akitoa ubani wa shilingi Milioni 2,000,000/- kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa familia ya marehemu alisema jamii na waswahili wote katika mwambao wa Afrika Mashariki wanafahamu mchango mkubwa wa Msanii Bi Kidude katika fani ya muziki wa taarabu.
Alisema Zanzibar imepata sifa kubwa katika Nyanja za Kimataifa kutokana na mchango wa wasanii kwa kueneza sanaa ya Taarabu iliyotoa fursa kwa baadhi ya watalii na wataalamu kuvitembelea Visiwa vya Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameitaka Familia ya Msanii Bi Kidude kuwa na moyo wa subra katika kipindi hichi kigumu cha msiba na kuwaeleza kwamba msiba huo sio wao peke yao.
“ Kwa kweli sisi sote tunampenda sana Bi Fatma Binti Baraka { Bi Kidude }. Lakini tuelewe kwamba Mwenyezi muungu anampenda zaidi na ndio maana akamuhitaji Bi Kidude,“ alinasihi Balozi Seif.
Naye Mmoja wa wana Familia hiyo, Bwana Haji Ramadhan Suwed Buda kwa niaba ya Familia ya Marehemu Bi Kidude ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mchango wake wa kuungana nao katika msiba huo.
Bwana Haji alisema hatua hiyo ya Serikali imeleta faraja kwao na kupunguza machungu ya msiba huo.
Msanii Gwiji wa sanaa ya Taarab asilia na ngoma ya Unyago Marehemu Bi Kidude aliyekadiriwa kufikia umri wa zaidi ya miaka 98, aliwahi kuolewa mara mbili, lakini hakupata Mtoto.
Mwenyezi Muungu ailaze roho ya marehemu Bi Kidude mahali pema.

MAZISHI YA BI KIDUDE PICHANI


Jeneza lenye mwili wa marehemu Bi Kidude likitolewa kwenye msikiti, ambako mwili wake uliswaliwa.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Seif Sharrif Hamad akiweka mchanga kwenye kaburi la marehemu Bi Kidude wakati wa mazishi yake yaliyofanyika jana Zanzibar.
Rais Jakaya Kikwete akiweka mchanga kwenye kaburi la marehemu Fatuma Binti Baraka'Bi Kidude' wakati wa mazishi yake yaliyofanyika jana Zanzibar.
Msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul 'Diamond' akiweka mchanga kwenye kaburi la marehemu Bi Kidude
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Sheni akiweka mchanga kwenye kaburi la marehemu Bi Kidude wakati wa mazishi yake yaliyofanyika jana Zanzibar.

Wednesday, April 17, 2013

WASEMAVYO WASANII KIFO CHA BI KIDUDE


BAADHI ya wasanii wa filamu na muziki nchini wameeleza kusikitishwa na kifo cha msanii mkongwe wa muziki wa taarab nchini, Fatuma Binti Baraka, maarufu zaidi kwa jina la Bi Kidude.
Wakizungumza na magazeti ya Burudani na Uhuru jana, wasanii hao walisema kifo cha msanii huyo mkongwe ni pigo kubwa katika tasnia ya taarab nchini.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Wilsoni Makubi alisema, kifo cha Bi Kidude ni pengo kubwa kwa wasanii kwa vile alikuwa akichukuliwa kuwa mfano wa kuigwa na wasanii.
Makubi alisema tasnia ya sanaa ilimtumia Bi Kidude katika sehemu mbili, moja katika muziki na nyingine katika filamu na kufanikisha kazi zao kuwa nzuri na za kuvutia.
Alisema msanii huyo alikuwa kiraka kwani kila alichoombwa kukifanya, alishiriki kikamilifu bila kuharibu kazi za wahusika na alijitolea kufanya kazi na wasanii wengi bila kujali aina ya kazi na umri wa wahusika.
Alisema pia kuwa, Bi Kidude alikuwa balozi wa wasanii katika nchi za nje kwa kuwa wengi waliifahamu Tanzania kupitia kazi zake na hivyo kuinufaisha kiutalii.
"Ukiangalia katika matamasha mengi yaliyokuwa yakifanyika Zanzibar kama vile ZIFF, watalii wengi walikuwa wakimfuata Bi Kidude," alisema Makubi.
Msanii nyota wa filamu nchini, Jacob Steven 'JB' alisema taarifa za kifo cha msanii huyo zilimshtua, lakini kwa vile ni kazi ya Mungu, haina makosa.
JB alisema wasanii wa Tanzania wanapaswa kujifunza mengi kupitia kwake ili kuuenzi mchango wake katika muziki wa taarab.
Mwanamuzi Judith Wambura, maarufu kwa jina la Lady JayDee, kupitia ukurasa wake wa twitter aliandika: "Mungu ni mwema na mapenzi yake yatimizwe kwa kuwa msanii huyo ameweza kufanikisha mengi katika uhai wake na hasa kuwa mfano kwa wasanii wengi."
Jay Dee alisema atamkumbuka msanii huyo kupitia wimbo wake wa 'Muhogo wa Jang'ombe', ambao aliuimba kwa mara ya pili na kuwa moja ya nyimbo zilizompatia umaarufu.
"Ukitaka kujua kama Bi Kidude alikuwa kipenzi cha watu na alisaidia mafanikio ya wasanii wengi, angalia waliofanya naye kazi jinsi kazi zilivyopata mafanikio," alisema Jay Dee.
Mkurugenzi wa kikundi cha Jahazi, Mzee Yussuf alisema, amesikitishwa na kifo cha mkongwe huyo na kumuombea mapumziko mema.
Alisema katika kumuenzi msanii huyo, atatayarisha wimbo mmoja
utakaoelezea wasifu wake na kazi zake.
Mkurugenzi wa kikundi cha taarab cha Wanawake cha Zanzibar, Maryam Mohammed Hamdan alisema, kifo cha Bi Kidude ni pigo zima kwa taifa kwa vile alikuwa kipenzi cha wengi.
Uongozi wa Tamasha la Sauti za Busara umesema, ilikuwa vigumu kwao kuamini taarifa za msiba wa msanii huyo kutokana na kuzushiwa kifo mara kwa mara.

BI KIDUDE HATUNAYE, KUZIKWA LEO Z'BAR


Na Aboud Mahmoud, Zanzibar
MSANII mkongwe wa fani ya muziki wa taarab nchini, Fatuma Binti Baraka, maarufu kwa jina la Bi Kidude amefariki dunia.
Bi Kidude alifariki dunia leo saa 6:45 mchana nyumbani kwa mtoto wa ndugu yake, maeneo ya Bububu, Zanzibar baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya msiba huo kuhamishiwa nyumbani kwake maeneo ya Rahaleo, mmoja wa wajukuu wa marehemu, Omar Ameir alisema, marehemu Bi Kidude alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa idi na sukari.
"Bi Kidude alikuwa akiugua kwa muda mrefu na kutibiwa katika hospitali mbalimbali hapa nchini. Mara ya mwisho alitibiwa katika hospitali ya KMKM,"alisema.
Kwa mujibu wa Ameir, mazishi ya Bi Kidude yanatarajiwa kufanyika kesho mchana kijiji kwake Kitumba, Wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.
Hali ya afya ya Bi Kidude ilianza kuzorota kuanzia mwishoni mwa mwaka jana na kusababisha alazwe katika hospitali ya Hindu Mandal, Dar es Salaam.
Wakati alipolazwa kwenye hospitali hiyo, watu wengi walikuwa wakipishana kwenda kumsalimia, wengine wakitoka nje ya nchi.
Jambo moja kubwa, ambalo Bi Kidude alikuwa akililaani vikali wakati huo ni taarifa za kuzushiwa kufariki dunia.
“Watu wamenizushia kufa na wewe hukuja kuniona, ulifikiri nimekufa? Mi mzima, si unaniona, cheki,”alisema Bi Kidude huku akiuvuta
mkono wa mwandishi wa makala hii kwa nguvu, akiuminya ‘kibaunsa’ kuonyesha nguvu za misuli yake, kwamba yeye yuko mzima.
Bi Kidude alilazwa kwenye hospitali hiyo kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya sukari, ambayo alikuwa akiugua kwa kwa muda mrefu, lakini yalimzidia kutokana na kukiuka taratibu za vyakula.
“Kweli nilikuwa naumwa, ngozi yote ilivuka hii, nilikonda sana, ila sasa Alhamdulillah mi mzima, naweza kuondoka,”alisema.
Muda wote, ambao Bi Kidude amekuwa akiugua, alikuwa akiuguzwa na watoto wa ndugu zake. Hakubahatika kuzaa.
Ndugu wote watatu, ambao ni wadogo zake Bi Kidude, walishafariki dunia. Alikuwa anakula matunda ya watoto wa ndugu zake hao, ambao ndio waliokuwa wakimlea.
Baada ya kutolewa katika hospitali hiyo, Bi Kidude hakuruhusiwa kufanyakazi yoyote ya saa. Alitakuwa kupumzika. Pia alipigwa marufuku na madaktari kuvuta sigara.
Bi Kidude alikuwa gwiji wa muziki katika Bara la Afrika, katika fani ya mwambao, ambayo hujulikana kwa jina la taarabu. Muziki huu ambao ni mchanganyiko wa vionjo kutoka nchi za Kiarabu na Kiafrika, umetikisa sana katika mwambao wa Afrika Mashariki, yaani Zanzibar, Mombasa, Lamu na kwingineko.
Marehemu Bi Kidude alizaliwa katika kijiji cha Mfagimarigo, Zanzibar katika familia ya watoto saba (7). Baba yake, Mzee Baraka alikuwa ni mfanyabiashara wa nazi.
Wakati wote wa uhao wake, hakuwa akifahamu tarehe halisi aliyozaliwa, isipokuwa alichojua ni kwamba, alizaliwa wakati rupia ikitumika kama fedha na kwamba ilikuwa kabla ya Vita Kuu ya Kwanza ya Ulaya.
Wataalamu wa mahesabu baada ya kupata taarifa hizo, walimpigia hesabu na kumkabidhi miaka yake kwamba ni zaidi ya miaka 100.
Bi Kidude alianza uimbaji tangu alipokuwa na umri wa miaka 10 na alijifunza kutoka kwa msanii mkongwe na aliyetamba enzi hizo, Sitti Binti Saad.
Wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakifika Zanzibar kwenda kumuona Sitti na kwa vile alikuwa karibu na Bi Kidude, yeye ndiye aliyewapeleka nyumbani kwake na kupata nafasi ya kumsikia akiwaimbia.
Alipokuwa na umri wa miaka 13, kwa mara ya kwanza alitoroka nyumbani kwao Zanzibar na kukimbilia Tanzania Bara. Alifanya hivyo
baada ya kulazimishwa kuolewa.
Hata hivyo, alipokuwa kigoli wa kutosha kuolewa, aliolewa japokuwa ndoa hiyo  haikudumu kutokana na manyanyaso aliyokuwa akiyapata. Hivyo aliamua kukimbilia kaskazini mwa Misri ikiwa ni katika miaka ya 1930.
Akiwa Misri, aling'ara katika fani yake ya uimbaji na uchezaji ngoma. Lakini ilipofika miaka ya 1940, aliamua kurudi nyumbani Zanzibar ambako aliendelea na shughuli zake za uimbaji.
Enzi za uhai wake, Bi Kidude hakuwa akitegemea kazi moja tu ya kuimba. Alikuwa akifanya biashara zingine kama vile kuuza 'wanja' na 'hina', ambavyo alivitengeneza mwenyewe.
Mkongwe huyo pia alikuwa mtaalamu wa matibabu kwa dawa za mitishamba. Zaidi ya hayo, alikuwa mwalimu mzuri wa 'Unyago' na aliwahi kuanzisha chuo chake. Aliwahi kutamba kuwa,
katika wanafunzi wake wote, hakuna aliyepata talaka kutoka kwa mumewe.
Marehemu Bi Kidude amewahi kutembelea nchi nyingi, ikiwa ni pamoja na Oman, Ufaransa, Hispania, Ufini, Ujerumani na Uingereza. Pia amewahi kupata tuzo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ya Tamasha la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF) 1999.
Mwaka jana, mkongwe huyo alipata tuzo ya WOMAX. Miongoni mwa nyimbo alizowahi kuimba na kumpatia umaarufu ni Muhogo wa Jang'ombe.
Hakuwahi kupata elimu nyingine zaidi ya Quraan.

BURIANI MANJU HAJI MOHAMED


HATIMAYE safari ya miaka 55 ya msanii nguli na mkongwe wa fani ya muziki wa taarab nchini, Haji Mohamed Omar ilikoma Jumatatu iliyopita baada ya kufariki dunia kutokana na ugonjwa wa sukari.
Marehemu Haji, ambaye alikuwa mkurugenzi wa kundi la East African Melody, alifariki dunia saa nne asubuhi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam, ambako alipelekwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu baada ya kutojisikia vizuri.
Mazishi ya Haji yalifanyika juzi Zanzibar na kuhudhuriwa na mamia ya watu, wakiwemo wasanii mbalimbali wa muziki huo.
Kifo cha Haji ni pengo kubwa katika muziki wa taarab, hasa ile ya kisasa. Licha ya kuwa mmoja wa waanzilishi wa kundi la East African Melody, alikuwa mtunzi na mwimbaji mzuri wa muziki huo.
Marehemu Haji ni uzao wa mwasisi wa taarab visiwani Zanzibar, hayati Sitti binti Saad na amewahi kupanga muziki katika nyimbo nyingi za East African Melody.
Haji amekuwa msanii wa pili wa kundi la East African Melody kupoteza maisha katika kipindi cha miezi minne iliyopita. Januari mwaka huu, msanii mwingine nyota wa kikundi hicho, Lamania Shaaban naye alipoteza maisha kutokana na ugonjwa wa sukari.
Kundi la East African Melody lilianzishwa 1990 nchini Oman. Miongoni mwa waasisi wa kundi hilo ni Haji, Lamania, Peter Dawo, Ashraf Mohamed, Mlamali Adam na Mahmoud Al-Alawi.
Waimbaji wa mwanzo wa kundi hilo ni pamoja na Zuhura Shaaban, Rukia Ramadhani, Sihaba Muchacho, Khadija Yussuf, Khadija Kopa na Othman Soud.
Marehemu Haji alianza kupata umaarufu baada ya kuibuka na kibao chake cha kwanza katika kundi hilo kinachojulikana kwa jina la Majamboz na Mavituz.
Kwa kawaida, marehemu Haji alikuwa mpole, lakini alikuwa mcheshi kwa mtu alizomzoea. Ni kiongozi aliyeweza kuwafanya wasanii wa East African waishi kama ndugu kwa kusaidiana kimaisha.
Wakati kundi hilo lilipohamishia maskani yake katika Jiji la Dar es Salaam likitokea Zanzibar, Haji ndiye aliyewashawishi viongozi wenzake kununua nyumba maeneo ya Magomeni Mapipa, Dar es Salaam na kuwa makao makuu yao.
Katika upande mmoja wa nyumba hiyo, waliishi wasanii wa kike na upande mwingine waliishi wasanii wa kiume. Nyumba hiyo pia ilitumika kwa ajili ya mazoezi ya kundi hilo.
Akizungumza na mwandishi wa makala hii nyumbani kwake mtaa wa Livingstone, Kariakoo, Dar es Salaam 2002, Haji alisema waliamua kuhamishia maskani yao Tanzania Bara kutokana na kuwa na idadi kubwa ya mashabiki.
Miongoni mwa nyimbo za East African Melody, ambazo marehemu Haji alishiriki kuzitayarisha ni pamoja na Kinyago cha Mpapure, Bure yako, Pata leo, Hatusemani hatuchekani, Halo yako, Kama wewe hakuna, Penzi, Kipo kinachonivutia.
Marehemu Haji pia ndiye mtunzi wa nyimbo za Taxi Bubu, Shecky lesi, Sorry kwa huyu siye, Mnikome na Joho la Mungu.
Mmoja wa viongozi wa kundi hilo, Mlamali amekiri kuwa, kifo cha Haji ni pengo jingine kubwa, ambalo itakuwa vigumu kuzibika baada ya kumpoteza msanii wao mwingine Lamania.
"Ni kweli vifo vya Lamania na Haji ni pengo kubwa kwa East African Melody, lakini hatuna budi kusonga mbele,"alisema.
Kwa mujibu wa Mlamali, kundi hilo kwa sasa litakuwa chini ya Peter Dawo, ambaye atarithi cheo cha ukurugenzi, akisaidia na Ashraf.
Marehemu Haji alisoma elimu ya msingi katika shule ya Vikokotoni na kuhitimu darasa la sita 1976. Alisoma masomo ya sekondari katika shule ya Forodhani na kumaliza 1980.
Alianza kujifunza muziki katika vikundi vidogo vya muziki huo vya Zanzibar kabla ya kujiunga na kikundi kikongwe cha Ikhwan Safaa kabla ya kutua East African Melody.

BREAKING NEEWSSSS. BI KIDUDE AFARIKI DUNIA



Habari tulizozipata hivi punde zimeeleza kuwa, msanii mkongwe wa muziki wa taarab nchini, Baraka Mohamed, maarufu kwa jina la Bi Kidude amefariki dunia.

Kwa mujibu wa habari hizo, Bi Kidude amefariki dunia saa sita mchana nyumbani kwake Zanzibar.

Habari zaidi kuhusu kifo cha mkongwe huyo wa taarab tutawaletea baada ya muda mfupi ujao.

Monday, April 15, 2013

BREAKING NEWSSSS, HAJI MOHAMED WA EAST AFRICAN MELODY AFARIKI DUNIA

 Habari zilizotufikia hivi punde zimeeleza kuwa, msanii mkongwe na muziki wa taraab wa  kikundi cha East African Melody,  Haji Mohamed 'Kijukuu cha Siti Bint Saad, amefariki dunia.

Kwa mujibu wa habari hizo, Haji amefariki dunia leo saa nne asubuhi  wakati akipelekwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam baada ya kuzidiwa na presha.

Taarifa zimeeleza kuwa, marehemu Haji  alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya sukari na presha kwa muda mrefu.

Kifo cha Haji kimetokea miezi michache baada ya msanii mwingine wa kundi hilo, Lamania Shaaban kufariki dunia kwa ugonjwa wa kisukari.

Mwili wa marehemu Haji ulitarajiwa kusafirishwa leo mchana kwa boti ya Azam Marine kupelekwa Zanzibar kwa ajili ya mazishi.

Mkurugenzi wa East African Melody, Hashim Salum amesema leo kuwa, alipata nafasi ya kuzungumza na marehemu asubuhi na kumwambia kwamba
alikuwa anakwenda hospitali kuonana na daktari wake.

Marehemu Haji ameacha mke na watoto watatu.
Mungu ailaze roho yake mahali pema.