KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Friday, September 27, 2013

ISHA: SIPENDI KUUMIZWA KIMAPENZI


KIONGOZI wa kikundi cha muziki wa taarab cha Mashauzi Classic, Isha Mashauzi amesema kamwe katika maisha yake hapendi kuumizwa kimapenzi na mwanaume.

Isha amesema anapoachana na mwanaume, huwa hageuki nyuma na kwamba mapenzi kwake ni kitu cha kupita.

"Nikiacha nimeacha, sipendi kuumizwa, kazi yangu mwenyewe inaumiza,"alisema Isha alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Ng'aring'ari kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha Clouds TV mwishoni mwa wiki iliyopita.

Isha amesema amewahi kutongozwa na wanaume wengi, lakini kutokana na msimamo alionao kimapenzi, wamebaki kuwa rafiki zake baada ya kuwaeleza ukweli wa mambo.

"Wapo zaidi ya wanaume wanne, ambao walinitongoza na kunitaka kimapenzi, lakini niliwaeleza wazi kwamba, kwa vile kila mmoja ana mkewe nyumbani, siwezi kujihusisha nao katika suala hilo. Hivi sasa ni rafiki zangu wakubwa, huwezi kuamini,"alisema.

Hata hivyo, Isha ametahadharisha kuwa, mwanamke anapoamua kumtolea nje mwanaume, anapaswa kuwa makini ili kuepuka kujiingiza katika matatizo.

Alisema wapo wanaume wanaopenda vibaya na wanaoweza kufanya lolote pale wanapokataliwa kimapenzi, ikiwa ni pamoja na kuua ama kujiua.

"Hata kama humpendi, mchukulie taratibu, usimweleze kwa pupa, wewe ni mwanadamu, siyo ng'ombe, hujui anakupenda vipi,"alisema mwanamama huyo, ambaye alianza kupata umaarufu katika muziki wa taarab alipokuwa kundi la Jahazi.

Isha amekiri kuwa, aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Jumanne Tevez, ambaye alipiga naye picha za video ya wimbo wake wa Nakupenda kwa dhati, lakini hawakuwahi kupata mtoto.

Anasema anajuta kumtambulisha Tevez kwa watu wengine kwa sababu baadhi yao walitumia nafasi hiyo kumtaka kimapenzi kwa lengo la kumkomoa.

Licha ya kuachana na Tevez baada ya mpenzi wake huyo wa zamani kuoa mwanamke mwingine, Isha amesema bado wanaendelea kuwasiliana na kuwa na urafiki wa kawaida.

"Hata mkewe tuna uhusiano mzuri na wakati mwingine huwa tunapigiana simu kujulikana hali, namwita wifi naye ananiita wifi,"alisema Isha.

Isha amesema katika maisha yake, kamwe hawezi kupigana na mwanamke mwenzake kwa ajili ya kugombania mapenzi. Alisema tabia hiyo imepitwa na wakati.

Ametoa mwito kwa wanawake wa Kitanzania kujenga utamaduni wa  kupendana na kukosoana badala ya kujengeana chuki bila ya sababu za msingi.

Amesema inapendeza mwanamke anapomuonea mwenzake wivu wa kimaendeleo kwa kufanya kile kilichomvutia kutoka kwa mwenzake hata kama atakuwa anamuiga.

Isha amesema licha ya mkurugenzi mwenzake wa Mashauzi Classic, Thabiti Abdul kuhamia kundi la Five Stars, bado amekuwa akiendelea kufanya maonyesho na kundi hilo.

"Thabiti bado tuko naye, anakuja mazoezini, anapiga kinanda na gita kwenye maonyesho, kwa ujumla bado tuko naye,"alisema.

Isha amesema kwa sasa kundi lake la Mashauzi Classic linajiandaa kuipua albamu mpya, itakayokuwa na nyimbo sita. Amesema albamu hiyo itajulikana kwa jina la Asiyekujua hakuthamini.
Albamu hiyo itakuwa ya pili kwa Mashauzi Classic tangu kundi hilo lilipoanzishwa miaka miwili iliyopita.

Albamu ya kwanza inajulikana kwa jina la Si bure una mapungufu, iliyofuatiwa na Viwavi Jeshi. Albamu hizo mbili zilikuwa na nyimbo nne kila moja.

No comments:

Post a Comment