KWA HABARI ZA MUZIKI WA TAARAB, WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL ramozaone@gmail.com

Monday, September 17, 2012

JOKHA KASSIM AKANA KUWAPIGA VIJEMBE MZEE YUSSUF NA LEILA RASHID


"KUPIGANA vijembe katika tungo za taarab hakujaanza leo wala jana, tangu enzi za marehemu Leila Khatib, ambaye alikuwa akirushiana maneno na Khadija Kopa."
"Sisi waimbaji chipukizi tumerithi kwao. Siwezi kushangaa kusikia mtu anampiga vijembe mwenzake kwenye nyimbo za taarab," ndivyo alivyoanza mazungumzo yake mwimbaji taarab mwenye sura na sauti yenye mvuto, Jokha Kassim,ambaye kwa sasa yupo katika kundi la T-Moto.
Jokha alitoa ufafanuzi huo kutokana na kuwepo kwa madai kuwa, nyimbo zake nyingi anaziomba zimelenga kuwapiga vijembe, mkurugenzi wa kikundi cha Jahazi, ambaye pia ni mumewe wa zamani, Mzee Yussuf na mkewe wa sasa, Leila Rashid.
Baadhi ya mashabiki wa muziki huo wanadai kuwa, tangu Jokha alipoachana na Mzee, amekuwa akitunga nyimbo zenye mwelekeo wa kumpifa vijembe mumewe huyo pamoja na mkewe Leila, ambaye pia ni mwimbaji wa Jahazi.
Mzee alibahatika kuzaa na Jokha mtoto mmoja wa kiume, anayejulikana kwa jina la Yussuf na waliwahi kufanyakazi pamoja katika makundi mbali mbali ya muziki huo.
Jokha alisema kwa kawaida, muziki wa taarab ni wa malumbano na majibizano na kwamba imekuwa ikifanyika hivyo tangu enzi na enzi.
Alisema tangu akiwa mdogo, waimbaji wengi wa muziki huo walikuwa wakiimba nyimbo za kujibimizana hivyo haoni ajabu kwa waimbaji wa sasa nao kufuata mkondo huo.
"Nakumbuka marehemu Leila Khatib alikuwa akipigana vijembe sana na Khadija Kopa. Lakini lengo lao halikuwa baya, ilikuwa ni njia fulani ya kuvuta mashabiki kwenye maonyesho yao,"alisema.
"Hivyo hata sisi tumerithi kutoka kwao hao, ambao tunaamini ni wakongwe kwetu na wanaheshimika kwenye tasnia ya muziki wa taarab,"alisisitiza Jokha.
Hata hivyo, mwimbaji huyo alisema si kweli kwamba nyimbo nyingi anazoimba zimewalenga Yussuf na Leila. Alisema lengo lake ni kufikisha ujumbe kwa jamii kuhusu masuala mbali mbali.
Jokha alisema majibizano kwenye taarab ni mambo ya kawaida na kwamba kufanya hivyo kunaleta changamoto kwa mashabiki na vikundi vya muziki huo.
Alisema kibao chake kipya kinachojulikana kwa jina la 'Domo la udaku' hakimlengi mtu yeyote kama baadhi ya mashabiki wanavyodai. Alisema mpangilio wa mashairi ya wimbo huo yamekuwa yakileta tafsiri mbaya, ambapo wengi wanaamini kuna mtu aliyekusudiwa.
Jokha alisema lengo lake katika kutunga wimbo huo ni kuielimisha jamii juu ya mambo mbali mbali kama ulivyo wajibu kwa msanii.
Mwimbaji huyo mwenye macho yenye mvuto pia alisema kwa sasa anajiandaa kuachia kibao kingine kipya, ambacho alitamba kwamba kitakuwa moto wa kuotea mbali.
Akizungumzia maisha yake ya sasa baada ya kujiunga na T-Moto, alisema mambo yanamwendea vizuri na kipaji chake kinazidi kuongezeka.
Alisema tayari wamesharekodi albamu inayoitwa 'Aliyeniumba hajakosea', ambayo imekuwa gumzo mkubwa kwa mashabiki wa muziki huo.
Jokha alisema baada ya albamu hiyo, wanatarajia kuipua albamu zingine mbili zitakazojulikana kwa majina ya Mimi staa na Domo la udaku.
Alizitaja baadhi ya nyimbo zitakazokuwemo kwenye albamu hizo kuwa ni Mwanamke hashuo na Wewe si daktari wa mapenzi.

No comments:

Post a Comment